1 Aprili 2022 - 19:12
Marekani yanunua kwa wingi mafuta ya Russia licha ya kudai imeyapiga marufuku

Licha ya kuweko amri ya rais wa Marekani, Joe Biden ya kupiga marufuku kuingizwa nchini humo mafuta kutoka Russia, lakini idara ya taarifa za nishati ya Marekani yenyewe imetangaza kuwa, uingizaji wa mafuta ya Russia nchini humo umeongezeka kwa asilimai 43 katika kipindi cha wiki moja iliyopita.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: limenukuu ripoti mpya ya Idara ya Taarifa za Nishati ya Marekani (EIA) ikitangaza kuwa, kiwango cha uingizaji wa mafuta ya Russia ndani ya Marekani kuanzia tarehe 19 hadi 25 mwezi ulioisha wa Machi kimeongezeka kwa asilimia 43 ikilinganishwa na wiki ya kabla yake.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, takwimu zinaonesha kuwa, kwa siku Marekani inaingia mapipa laki moja ya mafuta ghafi kutoka Russia. Ikumbukwe pia kuwa kwa mujibu wa taarifa rasmi, uingizaji wa mafuta ya Russia ulikuwa umedaiwa kupigwa marufuku katika wiki ya tarehe 19 hadi 25 Februari.

Lakini mwanzoni mwa mwezi ulioisha wa Machi, kiwango cha kuingizwa mafuta ya Russia nchini Marekani kimepanda kwa kiwango cha juu zaidi kuwahi kutokea katika mwaka huu wa 2022. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wastani wa mapipa laki moja na 48,000 ya mafuta ya Russia yamekuwa yakiingia nchini Marekani kila siku licha ya Joe Biden kuitangazia dunia kuwa amepiga marufuku kuingizwa mafuta ya Russia nchini Marekani.

Tarehe 8 mwezi ulioisha wa Machi, Joe Biden aliutangazia ulimwengu kuwa serikali yake huko Marekani imeanza kutekeleza marufuku ya kuingiza mafuta na kila kinachohusiana na masuala ya nishati kutoka Russia.

Wizara ya Hazina ya Marekani ilitangaza kuwa, mchakato wa kusimamisha uingizaji wa nishati ya Russia nchini humo utakamilika tarehe 22 mwezi huu wa Aprili. Nishati hiyo ni pamoja na mafuta, makaa ya mawe n.k. Shirika la habari la FARS pia limesema, bei ya mafuta imepanda vibaya katika historia ya Marekani tangu Biden alipotangaza kupiga marufuku kuingiza nishati kutoka Russia.

342/